Hot Posts

6/recent/ticker-posts

TIMU YA SIMBA IMEINGIA HATUA YA MAKUNDI YA MICHUANO YA KLABU BINGWA AFRIKA


Na Eleuteri Mangi, WUSM , Dar es Salaam 


Timu ya Simba imefuzu kuingia hatua ya makundi ya Klabu Bingwa Afrika kufuatia matokeo ya sare ya goli 1-1na timu ya Power Dynamo ya Zambia katika mchezo uliochezwa leo Oktoba 1, 2023 Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam.


Matokeo hayo yanaifanya Simba isonge mbele kutokana na kufaidika na goli la ugenini ambapo timu hizo zilitoka sare ya 2-2 katika mchezo uliochezwa nchini Zambia. 


 

Mgeni Rasmi katika mchezo huo, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Hamis Mwinjuma amesema mchezo wa soka umekuwa kwa kiwango kikubwa ambapo Tanzania kwa mara ya kwanza imeingiza timu mbili katika hatua ya makundi katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika.


"Nambari zinaongea, mpira wetu upo juu sana na mimi najiona mwenye bahati sana nikimsaidia Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan nikiwa katika nafasi hii ya Naibu Waziri na haya yanatokea, kismati cha Mama kinaendelea katika michezo" amesema Naibu Waziri Mwinjuma. 


Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Gerson Msigwa amesema Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anafurahishwa na timu zetu zinavyofanya vizuri katika mashindano ya kimataifa.


"Niliwaambia Mama hana mbambamba, goli la Mama linaanzia hatua ya makundi kila goli ni Sh. Milioni 5, Robo Fainali Milioni 10 na Nusu Fainali milioni 20" amesema Katibu Mkuu Msigwa.


Timu ambazo zimefuzu hatua ya makundi ni Simba baada ya kuwatupa nje ya michuano hiyo Power Dynamo ya Zambia na timu ya Yanga ambayo imewatupa nje ya michuano hiyo timu ya El Merreikh ya nchini Sudan.


Timu za Simba na Yanga sasa zinasubiri makundi ambayo yatapangwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) ili kuendelea na hatua ya robo fainali, nusu fainali na hatimaye fainali za Klabu Bingwa Afrika. 

Post a Comment

0 Comments