Kama ulidhani Simba inaiogopa Al Ahly ya Misri sahau, kwani mastaa tisa wa kikosi hicho cha Msimbazi wanaijua vyema timu hiyo na wamepewa kazi maalum ya kumalizana nayo hapo Oktoba 20 kwenye Uwanja wa Mkapa katika uzinduzi wa michuano mipya ya Africa Football League (AFL).
Mastaa hao wa Simba waliowahi kukutana na Al Ahly na kuwapelekea pumzi ya moto ni Aishi Manula, Mohamed Hussein, Shomary Kapombe, Kennedy Juma, Clatous Chama, John Bocco na Luis Miquissone, ambao walikutana nayo hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa misimu miwili tofauti.
Kocha mkuu wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ amethibitisha uwepo wa mastaa hao ni turufu muhimu kwenye mchezo huo na atawatumia kama silaha za kuimaliza Ahly lakini akasisitiza lengo lao ni kushinda na kuweka heshima.
“Wachezaji wetu wengi wana uzoefu na mechi za namna hii na hiyo ni faida kwa timu nzima.Tunaendelea na maandalizi ambapo lengo la kwanza ni kushinda tu,” aesema Robertinho.
Luis alirudi msimu huu akitokea Ahly ambayo ilimsajili mwaka 2021 baada ya kuitungua bonge la bao katika moja ya mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika, sasa unaambiwa jamaa amepania kuwaonyesha kwamba yeye ndiye yuleyule aliyewafunga wakati ule hadi wakamsajili.
Sambamba na wakali hao saba, wachezaji wapya ndani ya kikosi hicho, beki Che Malone na kiungo Fabrice Ngoma nao wanaijua vyema Ahly kwani waliwahi kukutana nayo kabla ya sasa.
0 Comments