Ubora wa beki Kouassi Yao umemuibua Kibwana Shomari aliyekiri kupata darasa kutoka kwa staa huyo huku akiweka wazi kuwa ni beki aliyekamilika kwenye kukaba na kushambulia.
Kibwana ambaye alikuwa panga pangua misimu miwili iliyopita kwa sasa anakaa benchi kumpisha Yao aliyejiunga na timu hiyo dirisha kubwa la usajili akitokea Asec Mimosas ya Ivory Coast.
Kibwana amesema; “Ni kweli sasa nasugua benchi nakubali kuzidiwa uwezo na Yao. Ni mchezaji mzuri ambaye ana uwezo mkubwa wa kukaba na kushambulia. Ana pumzi akipanda anawahi kurudi kuzuia mashambulizi na ana nguvu.
“Hilo limeniamsha na kunipa akili ya kuongeza ujuzi zaidi ili nirudi kwenye ushindani. Bado nina nafasi ya kucheza na nitafanya kwa ubora ili kumpa imani kocha kuwa hakosei kunipa nafasi ya kucheza.” amesema.
Kibwana amesema uwezo alionao Yao ni mkubwa amekuja kumpa elimu kuwa bado ana kazi kubwa ya kufanya ili kuongeza ubora wake na kujenga mwili ambao utampa nafasi ya kupambana na wachezaji wa aina zote bila kujali maumbile yao makubwa.
Katika msimu huu Yao tayari amekwishacheza kwa dakika 388 akicheza mechi tatu kwa dakika zote 90, huku mechi mbili akicheza dakika pungufu moja dakika 33 na nyingine dakika 85 kwenye mechi hizo amefunga bao moja na kutoa pasi tatu za mabao.
0 Comments