KIPA wa zamani wa Azam FC ambaye kwa sasa anakipiga KMC, Wilbol Maseke ni mchezaji asiyependa usafiri wa ndege, na anasema tukio ambalo lilifanya aingiwe na uoga ni hili:
.
“Ilikuwa 2022 tulikuwa tunakwenda Arusha, sasa kulitokea matukio ya ndege kuanguka nikamwambia kocha sipandi ndege akanibembeleza hadi nikakubali. Tukafika hadi uwanja wa ndege tumepanda vizuri tu, wachezaji mara nyingi tunapenda kukaa siti za nyuma kabisa.
.
“Nakumbuka ile ndege ilikuwa na abiria wa Kizungu wasiozidi watano. Mara tukaambiwa tufunge mikanda tukafunga baada ya dakika kadhaa likatoka tangazo lingine kuna tatizo kidogo limetokea tutapandishwa ndege nyingine. Matangazo ya Kingereza, mimi nikasimama nikatoa begi, wachezaji wenzangu wakaanza kucheka na kuniona nimechanganyikiwa.
.
“Nikawaambia ni kweli sijui sana Kiingereza ila nimeelewa, mara Wazungu wakachukua mabegi na kuanza kushuka ndipo wakaniamini. Baada ya muda fulani wakasema tatizo ilikuwa mlango wamerekebisha tunatakiwa kuendelea na safari, mimi nikakataa akaja meneja wa ndege kuniomba nikamkatalia, akaja kocha na meneja nikasimamia msimamo wangu, nikachwa na kurejea kambini.”
.
Anasema amesafiri peke yake na basi la timu zaidi ya mara 10 wenzake wakitumia usafiri wa anga. Hata hivyo anasema ipo siku atapanda tu ndege.
0 Comments