Mabosi wa Yanga wanakutana kufikiria watapitaje kwenye mechi sita za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Lakini mastaa wawili wenye heshima Jangwani wamesema kwa vile Hafiz Konkoni aliyesajiliwa kama mbadala wa Fiston Mayele ameshindwa kupiga kazi, angefyekwa mapema kwenye dirisha dogo ili aletwe mshambuliaji wa maana.
Kama hujui kwenye mabao 15 ambayo Yanga imefunga ni mawili pekee yaliyofungwa na washambuliaji halisi ambao ni Kennedy Musonda na Hafiz Konkoni.
Takwimu hizo zikawaibua kiungo mshambuliaji wa zamani, Sekilojo Chambua aliyesema katika dirisha dogo la usajili linalokuja lazima mabosi wao warudi sokoni kusaka mshambuliaji.
Chambua amesema; “Unajua ukweli ni kwamba bado hatujapata mtu kama Mayele (Fiston) nafahamu hatuwezi kupata mtu wa kariba yake, lakini timu ilikuwa inahitaji angalau kuona mtu ambaye atakuja na ubora wake na kuendelea kufunga.
“Nadhani viongozi wanatakiwa kurudi sokoni kutafuta mshambuliaji mpya, timu inahitaji mtu anayejua kufunga hiyo ndio kazi ya mshambuliaji, tunahitaji kuwa na mtu ambaye akipata nafasi tatu basi anaweza kufunga mbili au angalau moja.”
Wakati Chambua akiyasema hayo ligendi mwingine ambaye ni winga, Edibily Lunyamila amesema; “Timu inahitaji mshambuliaji hilo ndio jambo pekee lililosalia kwenye kikosi cha Yanga sasa, tunahitaji mshambuliaji anayejua kufunga awe anatumia muda mwingi kwenye eneo la hatari.
Via mwanaspoti
0 Comments