Mabondia Hassan Mwakinyo, Dullah Mbabe na Twaha Kiduku wameporoka kwenye ubora wa Tanzania katika kila uzani (pound for pound).Mbali na ubora wa Tanzania, Mwakinyo pia ameporoka kwenye uzani wake wa super welter duniani ambako sasa ni wa 106 kati ya mabondia 1893.
Bondia huyo aliyewahi kuingia kwenye 14 bora ya dunia mwaka 2019, ameendelea kuporomoka kutokana na kutopigana muda mrefu.
Japo mwenyewe amelieleza Mwanaspoti kwamba anaendelea kujifua kujiweka fiti, huenda kifungo cha mwaka mmoja alichopewa na Kamisheni ya ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC) kikamporomosha zaidi.
Ifikapo Aprili 24 mwakani bila kucheza bondia huyo ataondoshwa kwenye renki za mtandao wa ngumi za kulipwa wa dunia (Boxrec) ambazo bondia asipocheza kwa siku 365 anaondoshwa.
Pambano la mwisho la Mwakinyo lilikuwa dhidi ya Kuvesa Katembo aliloshinda kwa pointi Aprili 23 mwaka huu.
Septemba 29 aligomea pambano na Julius Indongo kwa kile ambacho alidai promota alikiuka makubaliano, jambo lililopelekea TPBRC kutangaza kumfungia mwaka mmoja na kulipa faini ya Sh1 milioni, ingawa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumbaro alikaririwa akieleza wizara itapitia upya adhabu hiyo.
Mbali na Mwakinyo, Kiduku na Mbabe pia wameporomoka kwenye ubora wa Tanzania katika kila uzani.
Kiduku ni wa 13 kutoka nafasi ya tano wakati Mbabe amekamata nafasi ya 36 kutoka ya 14 kwenye pound for pound, wakati kwenye uzani wao wa super middle, Kiduku ameendelea kuwa namba moja na Mbabe akiporomoka hadi nafasi ya nne kutoka ya pili aliyokuwa awali.
Via mwanaspoti
0 Comments