Kule (Algeria) nilimuona Mzamiru Yassin yuleyule ambaye wote tunamfahamu. Tulimpuuza na kisha tukampuuza. Lakini ameendelea kuwa muhimu katika kikosi cha Simba na timu ya taifa.
.
Wanabadilika makocha tu lakini nafasi yake ipo palepale. Wanabadilika wachezaji wenye vipaji tu katika nafasi zake, kuanzia Simba hadi timu ya taifa lakini yeye nafasi yake iko palepale.
.
Tunahitaji timu ya kina Mzamiru. Ni mfano. Uzuri wake ni kwamba siku hizi anajua kukaa na mpira na kupiga pasi kwa usahihi. Ni tofauti na zamani ambapo alikuwa anajua kukaba zaidi kuliko kukaa na mpira na kuuchukulia maamuzi sahihi.
.
Wakati lango la Stars likiwa majaribuni mchezaji mmoja wa Algeria alipata nafasi na kupiga shuti ambalo kama lingekwenda moja kwa moja lingeweza kuwa bao. Sospeter Bajana aliulaza mwili wake katika njia ambao mpira ungepita. Ukambabua na kurudi ulikotoka.Huyu naye Haimbwi sana kwa sababu hachezi Simba wala Yanga. Katika kikosi cha Taifa Stars pale Annaba alijitambulisha rasmi kwa mashabiki kuhusu kitu anachoweza kufanya uwanjani.
.
Ni shujaa. Ni aina ya wachezaji ambao wanaweza kuweka mguu sehemu ambayo inaweza kuvunjika. Wanaweza kuweka kichwa katika sehemu ambayo kinaweza kupasuka. Kwa namna anavyocheza, ataendelea kuitwa katika kikosi cha Stars mpaka kocha achoke.
- Edo Kumwembe.
0 Comments