💬 Wasiwasi wangu umemalizwa na jambo linaloitwa wakati. Wakati umetuonyesha kwamba Banda hakuwa mchezaji wa ajabu kama ilivyozungumzwa. Banda ni aina ya wachezaji ambao waliurudisha nyuma kidogo ubora wa Simba. Yeye pamoja na mwenzake Pape Sakho hawakuweza kuziba pengo la mchezaji kama Luis Miquissone pale alipoondoka.
Waliletwa kwa ajili ya kuziba pengo la Mmakonde lakini mpaka Mmakonde anarudi hakuna mchezaji aliyeweza kuziba pengo lake kirahisi. Muda mfupi alioutumia uwanjani alionekana kujijali zaidi mwenyewe kuliko timu. Ni hadithi ile ile ya mchezaji kama Larry Bwalya. Wakati Clatous Chama alipoondoka hakuweza kuibeba Simba mabegani kwake mpaka Chama akarudi na kuendeleza utawala wake.
Ndicho ambacho kimetokea kwa kina Banda na Miquissone. Baada ya kuitazama vizuri Simba hii nimegundua kwamba kama Miquissone akiendelea kujifua na kupambana na UBONGE alio nao huku akiwa fiti zaidi, basi kuna uwezekano mkubwa Simba ikarudi tena kwake pamoja na kwa rafiki yake Chama.” - Edo Kumwembe.
0 Comments